E-mail from Anonymous Feb.1(in Swahili)
Wed, 31 Jan 1996 08:14:47 +0300 (EAT)
Assalaam alaykum,
1. Mgomo wa wanafunzi Pemba bado unaendelea. Inakisiwa kama
asilimia 70 ya wanafunzi wanaendelea kugoma. Mapuri anasema SMZ
itazifunga skuli zinazogoma. Amesema kuwa wanafunzi wanaogoma
hawatachukuliwa hatua ila wale wanaowashawishi kugoma ndio
watachukuliwa hatua. Pemba kuna wanafunzi kama 60,000 kati ya
wanafunzi 150,000 wa Zanzibar nzima.
2. Wawakilishi wa CUF hawakuhudhuria semina ya Baraza la
Wawakilishi kwa siku ya pili. Bado Mwakilishi Mohamed Mula
hajaachiwa. Ahmed Seif yeye aliachiwa kwa dhamana ya Sh. 50,000.
Wamesema hawahudhurii mpaka mwenzao atakapoachiwa. Semina hiyo
inamalizika leo. Katika semina hiyo, katibu Mkuu, Wizara ya Katiba
na Sheria, Othman Masoud, jana alitahadharisha kuwa haki na kinga
za wawakilishi zilizoainishwa katika Katiba zinahitaji uangalifu
kuzitumia.
3. Mbunge mmoja wa NCCR (Musoma vijijini), Paul Ndobho, amesema kuwa
Mkapa asikwepe jukumu lake la kuhakikisha kuwa Pemba kuna usalama.
Amesema kuwa Ulinzi na Usalama ni sehemu ya mambo ya Muungano
yanayomhusu Mkapa. Aliyasema hayo kwenye semina ya Bunge
inayoendelea hapa Dar. Mbunge Ali Moh'd Shela (Kiwani) alishangaa
kuwa serikali ya Mkapa inasema inashughulikia masuala ya rushwa na
wasiolipa kodi lakini mpaka leo hakuna mla rushwa mkubwa hata mmoja
au anayekwepa kodi aliyeshikwa. Bunge la vyama vingi kwa kweli
linasisimua.
Mbunge Sanya (Mkunazini) alichekesha wabunge aliposema
alikuwa akipongezana na mwanafunzi wake wa kike kichochoroni
alipomuona askari polisi akiwa na sare zake za kiaskari huku akiwa
amevaa kanda mbili (ndara). Kilichowachekesha watu ni huko
kupongezana kichochoroni ingawa baadaye aliwatoa wasiwasi wenzake
kuwa hakuwa akifanya lolote baya na mwanafunzi wake huyo. Mbunge
Sanya alikuwa anakusudia kuwatetea askari polisi ili hali zao ziwe
nzuri.
Fatma Maghimbi (CUF, Chake) ameshangaa kuona kuwa nafasi za uwaziri
kwa wanawake zinazidi kupungua. Awamu ya 2 kulikuwa na mawaziri
wanawake wanne lakini sasa ni watatu tu. Alisema hiyo ni ishara
kuwa 2000 kutakuwa na wawili tu kama trend hiyo itaendelea.
Ndugu Philip Marmo (Mbulu) kachaguliwa Naibu Spika wa Bunge.
4. Walioshikwa na Majira Unguja wamehukumiwa kulipa faini ya Sh
30,000 au jela mwaka mmoja. Mbarouk Yusuf na Yohana Stanley ndio
wamehukumiwa hivyo. Wote wamelipa faini.
Samahani nimo harakani.
Tue, 30 Jan 1996 12:16:40 +0300 (EAT)
Assalaam alaykum,
Naona dhiki kubwa kuwa kila siku nawaelezea taarifa mbaya tu za
kuhusu nchini kwetu. Lakini kwa kweli hivyo ndivyo mambo yalivyo.
Jana nilikuwa nikisikiliza taarifa ya habari ya saa moja za usiku
ya Sauti ya Tanzania Zanzibar na hakuna hata habari moja iliyokuwa
nzuri: yote yalikuwa ni mambo ya siasa tena sio ya kufurahisha.
1. Watu watatu wamekamatwa Wete, Pemba kwa tuhuma za kutaka kulitia
moto jengo la Baraza la Wawakilishi lilioko mjini hapo. Watu hawa
walikamatwa na polisi baada ya kwisha kutupa bomu la petroli kwenye
jengo hilo na wakiwa na madebe mengine ya petroli. Moto uliwahiwa
na ukazimwa kabla ya kuleta madhara makubwa. Majina ya waliokamatwa
hayakutolewa.
2. Waziri Mkuu, Sumaye amesema malumbano kuhusu Uchaguzi Mkuu wa
Zanzibar yamalizwe kwani hayamsaidii chochote mwananchi wa kawaida.
Aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa semina ya siku 3 ya wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi. Wawakalishi wote wa CUF wameisusia semina
hiyo kupinga kukamatwa juzi kwa wawakilishi wenzao wawili, Ahmed Seif
(Utaani) na Mohamed salim Ali (Mkoani), huko Pemba.
3. Mbarouk Yusuf Khamis alifikishwa mahakamani jana kujibu shtaka
la kukamatwa na nakala ya gazeti la Majira la tarehe 27 Jan.,
bandarini Unguja akitokea Dar es Salaam.
4. Rais Mkapa ameziomba nchi wahisani kusaidia kuelimisha kuhusu
utamaduni wa vyama vingi ili wananchi waweze kuheshimu sheria na
serikali ya chama kilichoshinda. Aliyasema hayo kwenye mazungumzo
yake na Bibi Lynda Chalker, Waziri wa maendeleo ya nchi za nje wa
Uiengereza katika ziara yake ya siku tatu nchini. Akizungumzia
Zanzibar, aliwataka wahisani kuwaeleimisha wapinzani ukweli kwamba
ni kinyume cha sheria na maendeleo ya demokrasia kwa chama
kilichoshindwa kuleta vurugu badala ya kuwa mshiriki katika
maendeleo na serikali iliyopo madarakani. (Maoni yangu: Huyu ni
ngariba wa Kilwa - akata wenziwe kumbe yeye yu vivyo!! Maneno hayo
yalikuwa yaelekezwe kwa CCM kwanza).
5. Dr. Omar Ali Juma, Makamu wa rais, amewataka wanasiasa nchini na
nje ya nchi kuacha kuchochea uasi dhidi ya serikali ya Zanzibar na
kuutaka upinzani kuitambua serikali hiyo ili kuwepo mazungumzo
yatakayoleta suluhu, taarifa ya kutoka ofisi ya Makamu wa Rais
imeeleza. Aliyasema hayo kwenye mazungumzo na Balozi wa Denmark
nchini, Bw. Flemming Pederson. Dr. Omar alilalama kuwa wahisani
wanawasikiliza zaidi upande wa upinzani kuliko upande wa serikali
hivyo kufanya mvutano uendelee.
6. Mbunge Elizabeth Kasembe (Wanawake- CUF) atampeleka mahakamani
Mbunge, haji Juma Haji (CCM- Matemwe) kwa madai ya kumdhalilisha
kijinsia. Mbunge Elizabeth anadai kuwa Mbunge Haji alimwambia yeye
(Elizabeth) ni 'bibi wa wakubwa' ndio maana akachaguliwa kuwa
Mbunge. Kwa ushauri wa Spika Msekwa, na kwa kuwa tukio hilo
lilitokea nje ya Bunge, Mbunge Elizabeth anakusudia kuchukua hatua
za kisheria kwa mujibu wa sheria za Tanzania na sio kanuni za
Bunge. Tayari ameshamuona wakili Richard Rweyongoza kufungua
mashitaka.
7. Mgomo wa wanafunzi Pemba ulianza jana kwa wanafunzi kadhaa
kutohudhuria skuli ingawa wapo waliohudhuria kama kawaida. Wilaya
ya Wete na Mkoani ndizo zilizoongoza kwa mahudhurio mabaya. Kaimu
Afisa Mdhamini wa Wizara ya Elimu Pemba, Uledi Juma Wadi alisema
kuwa mgomo huo ulizikumba zaidi skuli za Jadida, Miti Ulaya,
Kizimbani na Utaani zote za Wete, Pemba. Kwa mfano Utaani yenye
wanafunzi 563, 407 hawakuhudhuria.
Mahudhurio pia yalikuwa mabaya kwa shule ya sekondari ya ufundi ya
Kengeja, skuli ya Mwambe na Ngwachani. Shamiani, Fidel Castro na
Chanjamjawiri hazikuathiriwa na mgomo huo wakati Ziwani na shule
nyengine za Chake Chake ziliathiriwa kiasi. Mgomo huo haufahamiki
utaendelea kwa siku ngapi.
Ah, yanatosha kwa leo!
Mon, 29 Jan 1996 13:27:46 +0300 (EAT)
Assalaam alaykum,
SMZ imemuweka ndani Mwakilishi wa Jimbo la Utaani, Wete, Pemba, kwa
tiketi ya CUF, Bw. Ahmed Seif Hamad. Alikamatwa juzi akitoka
msikitini kuswali Isha na Taraweikh. Mwakilishi mwengine wa Jimbo
la Mkoani (wa CUF), Bw. Mohamed Mula anasakwa na polisi.
Wote wawili wanashutumiwa kuhusika na kuchochea mgomo wa wanafunzi wa
Pemba nzima, uliopangwa kuanza leo, Jumatatu, kupinga uamuzi wa SMZ
uliofanywa juu ya baadhi ya wanafunzi wa Karume Technical College
(KTC) wanaotoka Pemba. Inasemekana kuwa wawakilishi hao walihutubia
mikutano ya kuwashawishi wazazi wasiwaruhusu watoto wao kwenda
shule kuanzia leo.
Wanafunzi 180 kutoka Pemba, walifukuzwa KTC walipoandamana kupinga
kukataliwa kuandikishwa kupiga kura katika uchaguzi uliopita.
Wizara ya Elimu baadaye iliamuriwa na mahakama kuwarudisha
wanafunzi hao wote. Wanafunzi 140 walirudishwa bila ya
masharti yoyote lakini 40 kati ya hao walikubaliwa wasome tu katika
vyuo vya Unguja lakini wajitafutie wenyewe vyakula na malazi.
Mgomo ulioitishwa, ambao umethibitishwa kuwa utaanza leo, na kuhusisha
shule zote za maandalizi, msingi, kati na sekondari, ni wa kupinga
uamuzi huo wa serikali.
Waziri wa Elimu, Bw. Ramadhani Mapuri, jana alitangaza radioni
kupinga mgomo huo na kuilaumu CUF kwa kuandaa mgomo huo. Wale
wanafunzi 140 waliorudishwa bila ya masharti, nao wamegoma kurudi
chuoni hadi hapo wenzao watakaporudishwa kusoma bila ya masharti.
Inasemekana kuwa hali ya kisiasa Pemba ni mbaya sana na jana askari
wa Polisi na FFU walionekana kukizunguka kituo cha Polisi cha Wete
(anachoshikiliwa Bw. Ahmed Seif Hamad), huku wakiwa na machela na
mabomu ya machozi.
Wakati huo huo, kuna tetesi kuwa walimu 12 wa KTC wanatarajiwa
"kuingwa" kufuatia shutuma ya kujihusisha na siasa (CUF) chuoni
hapo.
Sauti ya Tanzania Zanzibar, na RTD siku mbili hizi wanatoa
mazungumzo baada ya habari yanayowaponda CUF na wafuasi wao kwa
kudai ushindi wa Seif Shariff Hamad. Mazungumzo hayo yanadai kuwa
Uamuzi wa Tume za Uchaguzi, kwa mujibu wa Katiba, hauwezi kusailiwa
na yeyote yule hata Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hiyo ni katika
kujibu tahadhari ambayo viongozi wa CUF wamekuwa wakimpa Rais Mkapa
kuwa aiingilie kati suala hilo kwani kuna hatari ya kuzuka fujo
Z'bar.
Yarabi salama!
The letter from whom knows Zanzibar condition well.Oct.29.'95
E-mail from Tanzanian overseas.Oct.30.'95
E-mail from Tanzanian overseas .Nov.15.'95
E-mail from Anonymous Oct.31-Nov.3
E-mail from Tanzanian overseas Nov.19.'95
E-mail from Anonymous Nov.25
E-mail from Anonymous Nov.26
E-mail from Anonymous Dec.23
E-mail from Anonymous Jan.29
Zanzibar election Diary19-27 Oct.95
back to Home page